Tarehe ya kuandika: Katika
januari 1882, kwa Karl Marx na Friedrich Engels.
Tarehe ya kuchapishwa: Katika 1882.
Toleo hili: Marxists Internet Archive (marxists.org),februari 2013.
Chanzo cha Nakala: Karl Marks na Frederick Engels, Maelezo
y Chama cha Kikomunist, Moscow, Idara ya Maendeleo (1965).
Mchapo wa mwanzo wa Kirusi wa "Maelezo ya Chama cha Kikomunist", uliofasiriwa na Bakunin,[1] ulitokea mapema katika miaka ya sitini ya karne ya 19 katika nyumba ya kuchapia vitabu ya Kolokol[2] Wakati huo watu wa Magharibi waliweza kuuchukulia mchapo wa Kirusi wa “Maelezo" kama ni maandishi ya kuchekesha tu. Maoni kama hayo yasingewezekana kuwapo leo.
Jinsi nyendo za wafanya kazi zilivyokuwa zimeshikilia mahali padogo tu wakati huo (Desemba 1847) inaonyeshwa wazi wazi na sehemu ya mwisho ya "Maelezo" hayo: "Msimamo wa Wakomunist kuhusu vyama mbalimbali vya upinzani katika nchi mbalimbali." Hasa Urusi na Marekani hazipo hapo. Ulikuwa ni wakati ambapo Urusi ilikuwa ndiyo mlimbiko mkubwa wa mwisho wa nguvu za upingaji maendeleo wote wa Ulaya, ambapo wafanya kazi waliozidi katika Ulaya walikuwa wakihamia Marekani. Nchi zote mbili zilikuwa zikiipa Ulaya vitu visivyotengenezwa na pia zilikuwa ni masoko kwa kuuzia bidhaa za uchumi. Wakati huo nchi zote mbili kwa hivyo, kwa hali hii au nyingine, zikawa ndio nguzo kubwa za utaratibu ulioko Ulaya.
Jinsi gani mambo yalivyo tofauti kabisa leo! Hasa kuhama Ulaya kulisaidia maendeleo makubwa sana ya ukulima katika Marekani, ambao ushindani wake unaitikisa misingi yenyewe hasa ya wenye kumiliki mashamba wa Ulaya — wakubwa na wadogo. Isitoshe, kumeiwezesha Marekani kuzitumilia nguvu zake nyingi sana za uchumi kwa nguvu na kwa wingi mkubwa ambao lazima baada ya muda mchache uivunjilie mbali hali ya kuhozi uchumi wote ya Ulaya ya Magharibi, na hasa ya Uingereza, iliyopo mpaka sasa. Hali zote mbili zitaleta athari ya kithawra kwa Marekani yenyewe. Kidogo kidogo wakulima wenye kumiliki vipande vidogo vya ardhi na vya kiasi, msingi wa utaratibu wake wa kisiasa, wanaanza kuanguka katika mashindano dhidi ya wenye mashamba makubwa; papo hapo, umma mkubwa wa wafanya kazi na mkusanyiko wa rasilmali nyingi sana unakua kwa mara ya mwanzo katika sehemu zenye uchumi.
Na sasa Urusi! Wakati wa Thawra ya miaka 1848-1849 si wafalme wa Ulaya tu, lakini hata mabepari wa Ulaya pia, wameona kuwa hapana njia nyingine ya kuokoka kutokana na wafanya kazi, ambao ndio kwanza wanaanza kuamka, isipokuwa kutegemea msaada wa Urusi. Mfalme wa Urusi, alitangazwa kuwa ndiye mkuu wa wapingaji maendeleo wa Ulaya. Leo yeye ni mahabusi wa thawra, katika Gatchina[3], na Urusi imekuwa ndiyo kikundi cha mbele cha nyendo za kithawra katika Ulaya.
Kazi ya "Maelezo ya Kikomunist" ilikuwa ni kutangaza ukomeshaji ulio karibu sana usioweza kuepukika wa miliki ya sasa ya kibepari. Lakini katika Urusi tunakuta, ikikabiliana uso kwa uso na maendeleo makubwa ya kikepitalist yanayokua mbio mbio na miliki ya kibepari ya ardhi ambayo ndiyo kwanza ianzishwe, zaidi kuliko nusu ya ardhi yote inamilikiwa na wakulima kwa mujibu wa utaratibu wa obshchina[4]. Sasa swali lililoko ni kwamba: obshchina ya Kirusi, ingawa utaratibu huo wa kikale wa kumiliki ardhi kwa pamoja umepunguzwa sana umuhimu wake, inaweza kukiuka moja kwa moja kuingia utaratibu wa juu kabisa wa aina ya kumiliki ardhi, yaani ya kikomunist? Au kinyume cha hayo, lazima kwanza ipitie njia ile ile ya kuvunjika kama yalivyo katika mabadiliko ya kihistoria ya Magharibi?
Jawabu moja tu inayowezekana kutolewa kwa leo ni hii: pindi thawra ya Urusi itakuwa ndiyo ishara kwa thawra ya wafanya kazi katika Magharibi, ili kwamba zote mbili ziwe zinasaidiana, basi hali ya sasa ya kumiliki ardhi kwa pamoja katika Urusi yaweza kutumika kama ndio chanzo cha maendeleo ya kikomunist.
Karl Marks. F. Engels
London, tarehe 21 Januari, 1882
_________________________
[1] Bakunin, Mikhail Aleksandrovich (1814-1876) - mwanathawra na mwandishi wa Kirusi, mtaalamu wa mambo ya mawazo ya Narodnik (kundi la mabepari wadogo katika mwendo wa kithawra wa Kirusi) na mawazo ya anarchy (kutopendelea kuwapo utawala wo wote). Tangu mwaka 1840 alikuwa akiishi nchi za nje na kushiriki katika thawra ya 1848-1849 katika Ujerumani. Katika Jumuiya ya mwanzo ya Wafanya kazi wa Dunia, yaani International I ambayo yeye alikuwa ni mwanachama, aliyapinga kwa uchungu mawazo ya Marks, katika mwaka 1872 alifukuzwa kutoka katika Jumuiya hiyo kwa matendo yake ya kuugawa muungano. (Mteng.)
[2] Kolokol (Kengele) - Gazeti la kithawra la kidemokrasi la Kirusi lililokuwa likichapwa na Hertzen na Ogaryov katika 1857-1867. Мрака mwaka 1865 lilitokeza katika London na baadaye Geneva.
Tafsiri ya Kirusi ya "Maelezo ya Chama cha Kikomunist" inayotajwa hapa ilipigwa chapa Geneva katika mwaka 1869. (Mteng.)
[3] Hapa inakusudiwa hali iliyotokea baada ya kuuawa kwa mfalme wa Urusi, Aleksander II, tarehe 1 Machi, 1881 na wanachama wa jumuiya ya siri ya kisiasa Narodnaya Volya (Nia у a watu) ambapo mfalme mpya Aleksander III, kwa kuogopa matendo ya kithawra na ya ukatili yanayoweza kufanywa na wanachama wa Narodnaya Volya, alikwenda kujificha jumbani mwake huko Gatchina. (Mteng.) [4] Obshchina yaani komyuni ya kijijini. (Mteng.)